Scroll to Top
Attacks

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Sisi Chama cha Watu wenye Ualbinizm Tanzania (TAS) na Shirika la Under The Same Sun (UTSS) kwa pamoja tunalaani vikali ukatili uliofanywa dhidi ya Bi Ester Togolai Maganga (70) mwenye ualbinizm aliyekatwa kidole gumba cha mkono wa kulia huko Mlalo, Lushoto, mkoani Tanga.

Taasisi hizi mbili zinampa pole Maganga kwa maumivu aliyoyapata.

Mganga ambaye ni mjane alishambuliwa na watu watano wenye silaha usiku wa Disemba 08, 2015 akiwa nyumbani kwake alipokuwa akiandaa chakula cha usiku.

Watu hao walimkandamiza chini, wakamziba mdomo na macho na kisha walimkata kidole gumba chake na kutokomea gizani.

Huku damu zikimtiririka Maganga alikimbilia nje ya yumba yake alikokuwa akiishi peke yake na kupiga mayowe.

Majirani na wanakijiji walikusanyika na kutoa taarifa kwa Mwenye Kiti wa kijiji ambaye alimpeleka polisi ambao walimpeleka hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu.

Jeshi la polisi limewakamata watu wawili kuhusiana na mashambulizi hayo na linaendelea na kuwasaka wengine watatu waliokimbilia kusikojulikana.

Tunatoa wito kwa jamii ya Mlalo kumsaidia, kumlinda na kumfariji mjane Maganga.

Sisi TAS na UTSS vile vile tunatamka yafuatayo:

  • Tunakemea na kulaani vikali mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Said Mohammed (35) mwenye ualbinizm Mkuranga mjini Oktoba 21, 2015 siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu.
  • Tunajiuliza ukatili huu dhidi ya Watanzania wenzetu wasio na hatia utakwisha lini? Tunalitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na lile la Afrika Mashariki kujadili kwa kina tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu ili watu wenye ualbinizm waishi kwa amani nchini mwao.
  • Tunaiomba serikali itunge Sera za Kitaifa ya Watu wenye Ualbinizm ili masuala yao yashughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
  • Serikali sasa ichukue hatua madhubuti na utaratibu ulio wazi kupambanua kati ya Matatibu wa Tiba Asili ambao hutumia dawa asili kutibu maradhi na waganga wa kienyeji wanaopiga ramli, kujishirikisha na uchawi na kutumia viungo vya binadamu kuwatajirisha na kuwapa mafanikio ya kisiasa na mengineyo wateja wao. Hawa waganga wa kienyeji watafutwe, wakamatwe na shughuli zao zifungwe mara moja.
  • Jamii inayowazunguka watu wenye ualbinizm inapaswa kuwathamini na kuwalinda. Wote tunapaswa kutoa taarifa kwa vyombo husika kuhusu wageni kwenye maeneo yetu ambao hawana shughuli wala mwenyeji maalum.
  • Tunavitaka vyombo vya kisheria kuhakikisha kwamba wakatili hao wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
  • Tunaiomba serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kukomesha mauaji na ukatili unaoendelea kufanywa dhidi ya watu wenye ualbinizm.
  • Tunaiomba serikali ikishirikiana na wadau wa watu wenye ualbinizm na vyombo vya habari kufanya kampeni ya kukomesha mauaji ya watu wenye ualbinizm, ukataki viungo, utekaji nyara , ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya watu wenye hali hiyo ya kurithi.
  • Tunamuomba Mheshimiwa Rais atumbue majipu katika masuala ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbinizm kwa kuvipa nguvu zaidi vyombo husika kuwakamata wanunuzi na watumiaji wa viungo vya watu wenye ualbinizm.

Mwisho kwa pamoja tunampongeza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa utekelezaji kwa vitendo wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, kwa uteuzi wa Baraza lake la Mawaziri na kwa kuunda Wizara inayoongozwa na Naibu Waziri mwenye ualbinizm Mhe. Dkt. Abdallah Possi chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.

Taarifa hii imetolewa kwa ushirikiano wa TAS na UTSS Disemba 23, 2015.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na:

Nemes Temba                                                      Vicky Ntetema

Mwenyekiti wa TAS                                           Mkurugenzi Mtendaji – UTSS

Simu:  0767/0784/0658 874592                    Simu: 0756048487

Email: nemesct@gmail.com                            Email: vicky@utss.co.tz

 

 

 

 

Share and Enjoy

  • Facebook
  • Twitter
  • Delicious
  • LinkedIn
  • StumbleUpon
  • Add to favorites
  • Email
  • RSS
Like it? Share it!

Leave A Response

Email
Print